body{background: #ededed;margin:0;padding:0;}#menu_wrap{position:relative;margin-top:20px;margin-le

Monday, October 10, 2016

MOJA YA TUNGO ZANGU

    MALIZENI UCHUNGUZI
Wako wapi wa kauli,kelele kutupigia,
Wenye vyeo na manguli,wapi wameishilia,
Midomo yetu kufuli,nguvu imeshafifia
Malizeni uchunguzi, tufahamu mwisho wao.

Richimondi tafadhali,wapi ulikotokea,
Kama pepo za usuli.ulokuja tupepea’
Ulivuma kwa ukali,majanga kutuachia
Malizeni uchunguzi ,tufahamu mwisho wao

Dowan kaja na kauli,wote tukaipokea,
Mkataba wa tapeli,sahihi tikatilia
Ukosefu wa adili,hasara kwa Tanzania
Malizeni uchunguzi, tufahamu mwisho wao

Mara fisadi Bilali, wote tulimsikia
Alifia huko mbali,utata ukazagaa,
Tukafunika ukweli,tena tukanyamazia
Malizeni uchunguzi ,tufahamu mwisho wao.

Vijisenti kwa ukali,mbele akajitetea,
Tena mbele ya Jalali,umma ukashuhudia
Hekima ya udalali,nani kawapalilia
Malizeni uchunguzi, tufahamu mwisho wao

Waziri  akakubali,cheo akakiachia,
Karudi kwao Monduli, pesa kajitakasia ,
Akirudi mwanamwali,nchi mnampatia,
Malizeni uchunguzi, tufahamu mwisho wao

Upinzani nakubali,nao wamesaidia,
Mbunge wao tumbili,kwa ukweli kufichua,
Wakanuna mafahali, harufu ikazagaa
Malizeni uchunguzi ,tufahamu mwisho wao.

Madudu yaso asili, nasi  tumeshuhudia,
Tanzania ya adili, Escow akadakia,
Jalala lenye asali, wajanja kujichotea,
Malizeni uchunguzi, tufahamu mwisho wao.

Baba katulia tuli, kama anapotezea,
Kaja kutoa kauli, busara kaegemea.,
Kwetu midomo kufuli, tume wakajiundia
Malizeni uchunguzi, tufahamu mwisho wao.

Nchi haina ugali, ninyi mwajinenepea,
Uchaguzi wa halali, mbele unakaribia
Wanakuja madalali,pesa zetu kutumia
Malizeni uchunguzi , tufahamu mwiso wao


HII NI TUNGO MOJAWAPO YA SHAABAN ROBERT UNAWEZA KUIPITIA

VISIMA VYA
SHAABAN ROBERT

Na nianze kwa salaamu, salamu ni yangu jadi,
Pokea zangu salamu, usitie ukaidi,
Nyote kwangu ni muhimu, hakuna aliyezidi,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Hapa nitapaanzia, pengine kuelekea,
Tega sikio sikia, akilini kuyatia,
Moja mbili naingia, tayari kukuambia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Cha kwanza kufikirika, kisa mwana mfalume,
Mkuu mwana kataka, si binti bali kidume,
Waganga wakaitika, kwa kasi kama umeme,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Wakatoka wa kusini, magharibi wakafika,
Hata wa kasikazini, kipenga kiliwafika,
Mashariki sikioni, ngoma zilitetemeka,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Uponyaji kwa kafara, baraza lilitamka,
Ujinga kweli hasara, nchi iliharibika,
Waganga waso busara, miti mifugo kufyeka,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Shujaa Utubusara, akili alitumia,
Kuiondoa hasara, nchi ilokusudia,
Hakuyataka madhara, kama yaliyotokea,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Cha pili ni cha Adili, mgawo kisa kikuu,
Kisima chao ahali, na mambo yao makuu,
Wema kweli ni asali, twairamba wajukuu,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Dunia kamwe si mbaya, wala haina makucha,
Binadamu tu wabaya, twasemana kutwa kucha,
Wema hushinda ubaya, Adili hakuuacha,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Busara kubwa kichwani, haina katu faida,
Kama hauna moyoni, wema na njema ibada,
Utatoswa baharini, ndugu acha ya husuda,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Adili kashinda vita, kwa kutenda yalo mema,
Wema kwako nauleta, uwe baba naye mama,
Tenda pasi na kusita, imara mja simama,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Cha tatu binti Saadi, wasifu chaelezea,
Hiki kweli ni samadi, kipandwacho kinamea,
Giza linapokuzidi, kuchwa kuna karibia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Siti aliuza vyungu, mjini akaingia,
Maisha yale machungu, binti alivumilia,
Alitaka cha uvungu, kuimba aliingia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Siti alikuwa mwema, kwa watu wa rika zote,
Mema aliyoyachuma, yalifika nchi zote,
Siti kaacha alama, hakutenda kwa kitete,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Maisha kweli matendo, nini mja umetenda?
Singizi zaole vundo, waloshinda wametenda,
Epuka kuwekwa kando, kapambane tayashinda,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Rangi haina nafasi, katika kufanikiwa,
Mshipi utie tasi, kijana hujachelewa,
Hakuna jambo jepesi, liwezalo kimbiliwa,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Siti hakuwa Mtanga, watu wote tambueni,
Siti alitangatanga, mwisho yuko vitabuni,
Siti alitoa mwanga, nyayoze tufuateni,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Maji ya kisima hiki, matamu nakuambia,
Utamu haufichiki, Shabani katwandikia,
Jitenge na unafiki, heri itakufikia,
Visima vya shaabani, kamwe siwezifukia,

Nne ni maisha yake, humo ninaogelea,
Alitupenda wenzake, tawasifu katwachia,
Tuzifate nyayo zake, wema kuushangilia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Mapenzi kayamimina, Robert kasisitiza,
Alimpenda Amina, hata katika jeneza,
Alipenda wake wana, Shabani hakujikweza,
Visima vya shaabani, kamwe siwezifukia,

Alichapa zake kazi, kwa makini na stadi,
Aliheshimu wazazi, hakutenda ukaidi,
Aliwapenda wakazi, alitimiza ahadi,
Visima vya shaabani, kamwe siwezifukia,

Penzi bora katangaza, katika yake diwani,
Kisima chatuliwaza, mitungi kutwa vichwani,
Umpendaye  utamwaza, siku zote maishani,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Mapenzi kitu azizi, mja hilo litambue,
Usiitende ajizi, mwenzio mtamkie,
Mambo uyaweke wazi, wabukuzi wabukue,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Kisima kusadikika, njiani alikichimba,
Kwa wema katualika, wema ni la kwetu shamba,
Wavua pweza huvuka, katika wao mwamba,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Siku ya watenzi wote, shabani aliandika,
Bara visiwani kote, watenzi walizinduka,
Hawakuzicheza kete, siku wakaiitika,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

K’elelezo cha fasili, ni ubora wa Shabani,
Kimebaini vivuli, kweli ndoa ni kanuni,
Ameiandika kweli, fumbo kuu maishani,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Shabani taa angavu, nani asiyeijua,
Shabani mvumilivu, vitabu katwandikia,
Shabani bwana shupavu, popote aliingia,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia,

Utubora mkulima, kilimo alihimiza,
Alirudi himahima, mjini alikubeza,
Imara alisimama, uchumi kaukweza,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia.



Shaabani liandika, jitu jinga ni hasara,
Usiweke ushirika, hilo halina busara,
Zinduka dada kaka, badili zako fikra,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia.

Nitatia umakini, visimavye  kuvilinda,
Sintotia ufitini, mbegu bora kuipanda,
Aliimba ufukweni, kiswahili kukilinda,
Visima vya Shaabani, kamwe siwezifukia.

Sunday, October 9, 2016

MAMBO AMBAYO KIJANA HUTAKIWI KUYAFANYA...!
(1). Kuchagua Kazi.
Ni vigumu kupata Kazi ukiwa nje ya Kazi. Fanya Kazi uliyoipata upate Kazi unayoitaka.
(2). Kuchagua sehemu ya kuishi /kufanyia Kazi.
Maisha ni safari ndefu, maisha ni popote, si lazima kukaa mjini. Hauwezi kujua ni sehemu gan iliyobeba mafanikio yako. Chagua sehemu yenye FURSA na si yenye MAGHOROFA.
(3). Kuishi bila kuwa na malengo.
Maisha si bahat mbaya au nzuri. Maisha ni mipango, Maisha yanaongozwa na malengo. Vile ulivyo leo ni matokeo ya jinsi ulivyopanga jana, na vile unavyoishi leo ndivyo kesho yako itakavyokuwa. PANGA KESHO YAKO SASA.
(4). Maisha Ya kuiga.
Maisha yako si ya mwenzako, na ya maisha ya mwenzako si ya kwako. Si kila ukionacho ni lazima ufanye, chagua kipi cha kufanya na kipi cha kuacha. Kupitwa na jambo wakat mwingine sio USHAMBA ni BUSARA.
(5). Kuishi juu ya kipato chako.
Ishi kulingana na vile ulivyonavyo na si usivyonavyo. Kuwa na Busara katika MATUMIZI uepukane na MADENI yasiyo na ULAZIMA. RIDHIKA NA VILE ULIVYONAVYO.
(6).Kuishi bila AKIBA.
kuweka akiba ni TABIA sio kiwango kikubwa cha Pesa. Jenga tabia ya kujiwekea akiba. Haujui ni kipi kitakupata muda USIOTEGEMEA.
(7). Kuishi kwa kutegemea MSHAHARA.
Mshahara haujawahi kutosha na hautatosha kama ukishindwa kuishi chini ya kipato chako na kuwa na njia mbadala za kuinua kipato chako. JARIBU NJIA ZINGINE MBALI NA MSHAHARA.
(8).Kushindwa Kupangilia MATUMIZI ya Pesa.
Maamuzi yako ya pesa ndiyo yatajayoamua hali yako ya kiuchumi baadaye. Ni muhimu kujua kipi cha kununua, kwa wakat gani na kwa sababu gani. Jifunze kutofautisha kati ya liability (dhima) mfano: gari ya kutembelea na assets (kitegauchumi) mfano:nyumba au kiwanja . TUMIA PESA YAKO KUNUNUA ASSETS KULIKO LIABILITY.
(9).Kushindwa kutumia MUDA wako VIZURI.
Changamoto kubwa inayotukabili vijana ni kushindwa kujua namna ya kutumia vizuri muda. Tumia muda wako mwingi kujiendeleza ufahamu wako kwa kujisomea, kupanga malengo yako ya maisha, kujiuliza ni wapi ulikosea na nini ufanye ili urekebishe hayo makosa na muda mchache ufanye wa mapumziko na kufanya vitu vya kufurahisha akili yako kama kuangalia movie, mpira, kuingia kwenye mitandao ya kijamii Facebook, watsap n. k. Kumbuka muda ni rasilimali isiyoweza kurudishwa pindi unapopotea.
(10).Kuoa bila ya kujipanga kimaisha. (premature marriage).
Hii inawahusu wanaume, swala la kuoa ni pana sana na kila mtu ana vigezo vyake na mtazamo wake kufanikisha jambo hilo. Ila jambo la msingi ni hili, jiandae kwanza kiuchumi kabla hujaingiza majukumu mengine, unapoa ujue umekubali kusaidia upande wa mwanamke, upande wa familia yenu bila kusahau familia yako binafsi. Hata kama maisha ni kusaidiana na huyo utakayemuoa ila nafas yako kama mwanaume ITABAKI pale Pale. JIPANGE KWANZA.
MWISHO : UJANA NI KIPINDI AMBACHO NAKIFANANISHA NA KAMA SHAMBA LENYE UDONGO MZURI LINALOPOKEA KILA AINA YA MBEGU.. SASA ITATEGEMEA UNAPANDA NINI..!
*****Panda Chema Uvune Mema