MALIZENI UCHUNGUZI
Wako wapi wa kauli,kelele kutupigia,
Wenye vyeo na manguli,wapi wameishilia,
Midomo yetu kufuli,nguvu imeshafifia
Malizeni uchunguzi, tufahamu mwisho wao.
Richimondi tafadhali,wapi ulikotokea,
Kama pepo za usuli.ulokuja tupepea’
Ulivuma kwa ukali,majanga kutuachia
Malizeni uchunguzi ,tufahamu mwisho wao
Dowan kaja na kauli,wote tukaipokea,
Mkataba wa tapeli,sahihi tikatilia
Ukosefu wa adili,hasara kwa Tanzania
Malizeni uchunguzi, tufahamu mwisho wao
Mara fisadi Bilali, wote tulimsikia
Alifia huko mbali,utata ukazagaa,
Tukafunika ukweli,tena tukanyamazia
Malizeni uchunguzi ,tufahamu mwisho wao.
Vijisenti kwa ukali,mbele akajitetea,
Tena mbele ya Jalali,umma ukashuhudia
Hekima ya udalali,nani kawapalilia
Malizeni uchunguzi, tufahamu mwisho wao
Waziri akakubali,cheo
akakiachia,
Karudi kwao Monduli, pesa kajitakasia ,
Akirudi mwanamwali,nchi mnampatia,
Malizeni uchunguzi, tufahamu mwisho wao
Upinzani nakubali,nao wamesaidia,
Mbunge wao tumbili,kwa ukweli kufichua,
Wakanuna mafahali, harufu ikazagaa
Malizeni uchunguzi ,tufahamu mwisho wao.
Madudu yaso asili, nasi
tumeshuhudia,
Tanzania ya adili, Escow akadakia,
Jalala lenye asali, wajanja kujichotea,
Malizeni uchunguzi, tufahamu mwisho wao.
Baba katulia tuli, kama anapotezea,
Kaja kutoa kauli, busara kaegemea.,
Kwetu midomo kufuli, tume wakajiundia
Malizeni uchunguzi, tufahamu mwisho wao.
Nchi haina ugali, ninyi mwajinenepea,
Uchaguzi wa halali, mbele unakaribia
Wanakuja madalali,pesa zetu kutumia
Malizeni uchunguzi , tufahamu mwiso wao
No comments:
Post a Comment